Muzale, Henry R. T.2016-09-072016-09-072009Muzale, H.R.T., Changamoto Za Mawasiliano Kwa Viziwi Katika Tanzania. Kiswahili, 72(1).http://hdl.handle.net/20.500.11810/3653Full text can be accessed at http://www.ajol.info/index.php/ksh/article/view/79052Viziwi ni moja kati ya makundi ya watu wenye ulemavu wanaohitaji huduma maalumu, hasa shuleni. Ingawa matatizo ya kiziwi yako kwenye maumbile ya mwili wake, athari za ulemavu huo haziko katika mwili kwa maana ya kumsababishia maumivu, kama walivyo watu wenye aina nyingine za ulemavu. Matatizo aliyo nayo kiziwi humkwaza katika mawasiliano katika mazingira anamoishi na hivyo kumwathiri kwa njia nyingine mbalimbali katika nyanja za elimu, mahusiano na maendeleo ya kijamii. Aidha, kwa kuwa matatizo ya viziwi ni ya kimawasiliano, na kwa hiyo hayaonekani kwa macho, viziwi wamekuwa wakikabiliwa na tatizo la kusahaulika katika utoaji wa huduma, kama mojawapo ya makundi ya wanafunzi wanaohitaji msaada maalumu wa kielimu. Athari za mwenendo huu zinaweza kuonekana bayana kutokana na hali za viziwi kuanzia elimu ya awali hadi elimu ya juu, na hata katika maisha kwa jumla. Makala haya yanalimulika suala hili kwa undani, ikiwa ni matokeo ya utafiti alioufanya mwandishi pamoja na kujihusisha kwake na jamiii ya viziwi kwa muda mrefu. Kwa hiyo, lengo kuu la makala haya ni kubainisha hali halisi ya maisha ya jamii ya viziwi uhusiana na vikwazo vya mawasiliano vinayowakabili, hasa shuleni. Ili kutimiza lengo hilo, makala yanabainisha msingi mkuu na chimbuko la vikwazo hivyo. Msingi huo mkuu, ambao ni chimbuko la vikwazo ni mfumo wa elimu uliopo ambao unakazia matumizi ya lugha ya Kiswahili na Kiingereza kama lugha za kufundishia bila kuzingatia mahitaji muhimu ya wanafunzi viziwi. Makala yanachambua pia kasoro za mfumo wa mawasiliano darasani pamoja na matumizi ya ubao, ambavyo hukumbatia lugha za mazungumzo (Kiswahili na Kiingereza) na kuitelekeza lugha ya alama ambayo ndilo tegemeo kuu la wanafunzi wa aina hii. Kwa njia hiyo, makala haya yanachambua asili, aina na athari za vikwazo hivyo vya mawasiliano vinavyoikabili jamii ya viziwi kuanzia kwenye familia hadi shuleni. Ili kutoa mwanga wa kutosha wa masuala hayo, makala yanavinjari pia aina za uziwi, mahitaji ya kila kundi la viziwi, na athari za changamoto zilizopo kwa maisha ya kiziwi. Hayo yanabainishwa kwa kuchambua hali halisi ya madarasa wanakosoma wanafunzi viziwi na mbinu za ufundishaji zilizopo. Kwanza tunaangalia hali halisi ya darasa lenye watoto viziwi pekee katika shule za msingi, ambako Kiswahili hutumika, na kisha darasa la elimu-mjumuiko katika ngazi ya sekondari ambako Kiingereza hutumika. Kwa hiyo, pamoja na kukomaa kwa matumizi ya Kiswahili kama lugha ya kufundishia katika elimu ya msingi, makala yanabainisha ni kwa kiwango gani wanafunzi viziwi wanafaidika au wanaathirika na mifumo ya elimu na mawasiliano iliyopo nchini Tanzania.swChangamoto za Mawasiliano kwa Viziwi katika TanzaniaJournal Article, Peer Reviewed